Mfuko wa Pensheni wa PSPF umeendelea
kuboresha maisha ya wanachama wastaafu kwa kuwawezesha kupata mkopo kupitia
Benki ya Posta Tanzania.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa
mfuko huo Bw. Adam Mayingu wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini
Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya mfuko kwa miaka 15 tangu ulipoanzishwa.
Mayingu alifafanua kuwa mpaka sasa
zaidi ya shilingi bilioni 13 zimetumika kuwakopesha wastaafu wa PSPF wapatao
4,097 kwa lengo la kuwasaidia kwenye shughuli zao mbalimbali za maendeleo.
“PSPF ni mfuko wa kwanza nchini kuingia
mkataba na Benki ya Posta ambapo wanachama wastaafu wa mfuko wanaweza kupata
mkopo na mpango huu ulizinduliwa rasmi Juni 2014.”
Akieleza zaidi mafanikio ya mfuko huo
Mayingu alisema kuwa takwimu za Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya
Hifadhi ya Jamii (SSRA) zinaonyesha Mfuko wa PSPF una idadi kubwa ya wastaafu
na wategemezi kuliko mifuko mingine ambapo kwa miaka kumi sasa unahudumia
wastaafu na wategemezi wapatao 53,000 na kiasi cha trilioni 2.83 zimelipwa kwa
wanachama wake.
Aidha Mayingu aliongeza kuwa PSPF
wameweza kupata tuzo za kitaifa na kimataifa kutoka kwa wadau mbalimbali wa
hifadhi ya jamii ambao wametambua mchango wa mfuko huo katika kuboresha maisha
ya wanachama wake na kuchangia maendeleo ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari
(MAELEZO) Bw. Assah Mwambene ameupongeza Mfuko wa PSPF kwa kutoa mafao bora na
kwa wakati na kuwataka waendelee kuboresha huduma zao ili wanachama waweze
kunufaika zaidi.
Akitoa rai kwa waandishi wa habari Mwambene
amesema wanapaswa kuhakikisha wanaandika habari zitakazowasaidia watanzania
kuelewa mambo mbalimbali hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa katiba mpya badala ya
kukazania habari zisizokuwa na tija kwa jamii.
Source: MAELEZO
No comments:
Post a Comment