Hospitali ya Bugando imepunguza gharama za upasuaji wa moyo kutoka kati ya shilingi milioni tatu hadi kufikia shilingi elfu hamsini tu.
Hospitali ya rufaa Bugando iliyopo jijini mwanza imepunguza gharama za upasuaji wa moyo, kutoka kati ya shilingi milioni tatu hadi nane ilizokuwa inawatoza wagonjwa kwa upasuaji mkubwa na mdogo hadi kufikia shilingi elfu hamsini tu ili kuwawezesha wananchi wengi wasio na uwezo wa kumudu gharama hizo kunufaika na matibabu hayo.
Mkuu wa idara ya upasuaji wa moyo na kifua katika hospitali ya rufaa Bugando Prof. William Mahalu amessema kutokana na ukubwa wa tatizo la ugonjwa wa moyo, zaidi ya watoto 20 wanaopata huduma ya kliniki katika hospitali hiyo pamoja na watu wazima 25 wamekuwa kila mwezi wakigundulika kusumbuliwa na tatizo la moyo, ambapo mwaka huu watoto 10 wamegundulika na tatizo hilo na watoto sita wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa haraka.
Daktari bingwa wa kitengo cha upasuaji wa moyo kwa watoto katika hospitali hiyo Dk. Godwin Sharau pamoja na kuzishukuru taasisi za nje ya nchi, wadau na marafiki wa hospitali ya rufaa Bugando waliosaidia operesheni za moyo kufanikiwa kwa gharama nafuu kabisa, amesema mwaka huu lengo ni kuwafanyia operesheni wagonjwa 100 na miaka mitatu ijayo ni kufikia wagonjwa 250 kwa mwaka.
Mkuu wa wilaya ya Kwimba Selemani Mzee amesema huduma hiyo inayofanywa na idara ya upasuaji wa moyo na kifua inapaswa kuwafikia wananchi wengi hususani wa vijijini ambao pamoja na kusumbuliwa na tatizo hilo lakini wanahofia gharama kubwa ya matibabu, huku mzazi wa mtoto Lukaiya Shaban Bw. Shaban Juma Ramadhan ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji wa moyo na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo katika hospitali hiyo akishukuru kwa huduma hiyo.
Upasuaji wa moyo katika hospitali ya rufaa Bugando ulianza miaka saba iliyopita, ambapo hadi kufikia mwaka jana 2014, hospitali hiyo ilikuwa na jumla ya wagonjwa 769 waliokuwa wakingoja kufanyiwa upasuaji, aidha katika kipindi hicho watoto 44 walipelekwa Israel, 38 walitibiwa katika hospitali hiyo – ambapo 14 walifanyiwa upasuaji na madakatari bingwa wa moyo kutoka Australia na wengine 24 walifanyiwa upasuaji na timu ya madakatari wa hospitali ya Bugando.
No comments:
Post a Comment